26

1 T´aa Siin Miim. (T´.S.M.)
2 Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha.
3 Huenda labda ukajikera nafsi yako kwa kuwa hawawi Waumini.
4 Tunge penda tungeli wateremshia kutoka mbinguni Ishara zikanyenyekea shingo zao.
5 Wala hauwafikii ukumbusho mpya kutoka kwa Arrahman ila wao hujitenga nao.
6 Kwa yakini wamekanusha; kwa hivyo zitakuja wafikia khabari za yale waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha.
7 Je! Hawakuiona ardhi, mimea mingapi tumeiotesha humo, ya kila namna nzuri?
8 Hakika katika haya zipo Ishara. Lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.
9 Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
10 Na Mola wako Mlezi, alipo mwita Musa, akamwambia: Fika kwa watu madhaalimu,
11 Watu wa Firauni. Hawaogopi?
12 Akasema: Hakika mimi nachelea wasinikanushe.
13 Na kifua changu kina dhiki, na ulimi wangu haukunjuki vyema. Basi mtumie ujumbe Harun.
14 Na wao wana kisasi juu yangu, kwa hivyo naogopa wasije kuniuwa.
15 Akasema: Siyo hivyo kabisa! Nendeni na miujiza yetu. Hakika Sisi tu pamoja nanyi, tunasikiliza.
16 Basi mfikieni Firauni na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
17 Waachilie Wana wa Israili wende nasi.
18 (Firauni) akasema: Sisi hatukukulea wewe utotoni, na ukakaa kwetu katika umri wako miaka mingi?
19 Na ukatenda kitendo chako ulicho tenda, nawe ukawa miongoni mwa wasio na shukrani?
20 (Musa) akasema: Nilitenda hayo hapo nilipo kuwa miongoni mwa wale walio potea.
21 Basi nikakukimbieni nilipo kuogopeni, tena Mola wangu Mlezi akanitunukia hukumu, na akanijaalia niwe miongoni mwa Mitume.
22 Na hiyo ndiyo neema ya kunisumbulia, na wewe umewatia utumwani Wana wa Israili?
23 Firauni akasema: Na nani huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote?
24 Akasema: Ndiye Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi ni wenye yakini.
25 (Firauni) akawaambia walio mzunguka: Hamsikilizi?
26 (Musa) akasema: Ndiye Mola wenu Mlezi, na Mola Mlezi wa baba zenu wa kwanza.
27 (Firauni) akasema: Hakika huyu Mtume wenu aliye tumwa kwenu ni mwendawazimu.
28 (Musa) akasema: Ndiye Mola Mlezi wa Mashariki na Magharibi na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi mnatia akilini.
29 (Firauni) akasema: Ukimfuata mungu mwengine asiye kuwa mimi, basi bila ya shaka nitakufunga gerezani.
30 Akasema: Je! Ijapo kuwa nitakuletea kitu cha kubainisha wazi?
31 Akasema: Kilete basi, kama wewe ni katika wasemao kweli.
32 Basi akaitupa fimbo yake, mara ikawa nyoka wa kuonekana dhaahiri.
33 Na akautoa mkono wake, na mara ukawa mweupe kwa watazamao.
34 (Firauni) akawaambia waheshimiwa walio mzunguka: Hakika huyu ni mchawi mtaalamu.
35 Anataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake. Basi mna shauri gani?
36 Wakasema: Mpe muda yeye na nduguye na uwatume mijini wapigao mbiu ya mgambo.
37 Wakuletee kila mchawi bingwa mtaalamu.
38 Basi wakakusanywa wachawi wakati na siku maalumu.
39 Na watu wakaambiwa: Je! Mtakusanyika?
40 Huenda tutawafuata wachawi wakiwa wao ndio watakao shinda.
41 Basi walipo kuja wachawi wakamwambia Firauni: Je! Tutapata ujira tukiwa sisi ndio tulio shinda?
42 Naam! Na hakika mtakuwa katika watu wa mbele.
43 Musa akwaambia: Tupeni mnavyo taka kutupa.
44 Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa nguvu za Firauni hakika sisi hapana shaka ni wenye kushinda.
45 Musa tena akatupa fimbo yake, nayo mara ikavimeza walivyo vizua.
46 Hapo wachawi walipinduka wakasujudu.
47 Wakasema: Tunamuamini Mola Mlezi wa walimwengu wote.
48 Mola Mlezi wa Musa na Harun.
49 (Firauni) akasema: Je! Mmemuamini kabla sijakuruhusuni? Bila ya shaka yeye basi ndiye mkubwa wenu aliye kufunzeni uchawi. Basi mtakuja jua! Nitakata mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakubandikeni misalabani nyote.
50 Wakasema: Haidhuru, kwani sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi.
51 Hakika sisi tunatumai Mola wetu Mlezi atatusamehe makosa yetu, kwa kuwa ndio wa kwanza wa kuamini.
52 Na tulimuamrisha Musa kwa wahyi: Nenda na waja wangu wakati wa usiku. Kwa hakika mtafuatwa.
53 Basi Firauni akawatuma mijini wapiga mbiu za mgambo.
54 (Wakieneza): Hakika hawa ni kikundi kidogo.
55 Nao wanatuudhi.
56 Na sisi ni wengi, wenye kuchukua hadhari.
57 Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem,
58 Na makhazina, na vyeo vya hishima,
59 Kadhaalika; na tukawarithisha hayo Wana wa Israili.
60 Basi wakawafuata lilipo chomoza jua.
61 Na yalipo onana majeshi mawili haya, watu wa Musa wakasema: Hakika sisi bila ya shaka tumepatikana!
62 (Musa) akasema: Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu Mlezi. Yeye ataniongoa!
63 Tulimletea wahyi Musa tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana, na kila sehemu ikawa kama mlima mkubwa.
64 Na tukawajongeza hapo wale wengine.
65 Tukawaokoa Musa na walio kuwa pamoja naye wote.
66 Kisha tukawazamisha hao wengine.
67 Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara; lakini wengi wao si katika wenye kuamini.
68 Na kwa hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
69 Na wasomee khabari za Ibrahim.
70 Alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini?
71 Wakasema: Tunaabudu masanamu, daima tunayanyenyekea.
72 Akasema: Je! Yanakusikieni mnapo yaita?
73 Au yanakufaeni, au yanakudhuruni?
74 Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo.
75 Je! Mmewaona hawa mnao waabudu-
76 Nyinyi na baba zenu wa zamani?
77 Kwani hakika hao ni adui zangu, isipo kuwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
78 Ambaye ndiye aliye niumba, na Yeye ndiye ananiongoa,
79 Na ambaye ndiye ananilisha na kuninywesha.
80 Na ninapo ugua ni Yeye ndiye anaye niponesha.
81 Na ambaye atanifisha, na kisha atanihuisha.
82 Na ambaye ndiye ninaye mtumai kunisamehe makosa yangu Siku ya Malipo.
83 Mola wangu Mlezi! Nitunukie hukumu na uniunganishe na watendao mema.
84 Na unijaalie nitajwe kwa wema na watu watakao kuja baadaye.
85 Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema.
86 Na umsamehe baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni mwa wapotovu.
87 Wala usinihizi Siku watapo fufuliwa.
88 Siku ambayo kwamba mali hayato faa kitu wala wana.
89 Isipo kuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi.
90 Na Pepo itasogezwa kwa wachamngu.
91 Na Jahannamu itadhihirishwa kwa wapotovu.
92 Na wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwaabudu
93 Badala ya Mwenyezi Mungu? Je! Wanakusaidieni, au wanajisaidia wenyewe?
94 Basi watavurumizwa humo wao na hao wakosefu,
95 Na majeshi ya Ibilisi yote.
96 Watasema, na hali ya kuwa wanazozana humo:
97 Wallahi! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio dhaahiri,
98 Tulipo kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
99 Na hawakutupoteza ila wale wakosefu.
100 Basi hatuna waombezi.
101 Wala rafiki wa dhati.
102 Laiti tungeli pata kurejea tena tungeli kuwa katika Waumini.
103 Hakika katika haya ipo Ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.
104 Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
105 Kaumu ya Nuhu waliwakadhibisha Mitume.
106 Alipo waambia ndugu yao, Nuhu: Je! Hamchimngu?
107 Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
108 Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit´iini mimi.
109 Na sikutakini juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
110 Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit´iini mimi.
111 Wakasema: Je! Tukuamini wewe, hali wanao kufuata ni watu wa chini?
112 Akasema: Nayajuaje waliyo kuwa wakiyafanya?
113 Hisabu yao haiko ila kwa Mola wao Mlezi, laiti mngeli tambua!
114 Wala mimi si wa kuwafukuza Waumini.
115 Mimi si cho chote ila ni Mwonyaji wa dhaahiri shaahiri.
116 Wakasema: Ikiwa huachi, ewe Nuhu, bila ya shaka utapigwa mawe.
117 Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikanusha.
118 Basi hukumu baina yangu na wao kwa hukumu yako, na uniokoe mimi na walio pamoja nami, Waumini.
119 Kwa hivyo tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye katika marikebu iliyo sheheni.
120 Kisha tukawazamisha baadaye walio bakia.
121 Hakika katika haya ipo Ishara, lakini si wengi wao walio kuwa Waumini.
122 Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
123 Kina A´d waliwakanusha Mitume.
124 Alipo waambia ndugu yao, Hud: Je! Hamchimngu?
125 Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
126 Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit´iini mimi.
127 Wala sikutakeni juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
128 Je! Mnajenga juu ya kila mnyanyuko kumbusho la kufanyia upuuzi?
129 Na mnajenga majengo ya fakhari kama kwamba mtaishi milele!
130 Na mnapo tumia nguvu mnatumia nguvu kwa ujabari.
131 Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit´iini.
132 Na mcheni aliye kupeni haya mnayo yajua.
133 Amekupeni wanyama wa kufuga na wana.
134 Na mabustani na chemchem.
135 Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Kubwa.
136 Wakasema: Ni mamoja kwetu, ukitupa mawaidha au hukuwa miongoni mwa watoao mawaidha.
137 Haya si chochote ila ni mtindo wa watu wa tokea zamani.
138 Wala sisi hatutaadhibiwa.
139 Wakamkanusha; nasi tukawaangamiza. Hakika bila ya shaka katika haya ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
140 Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
141 Kina Thamud waliwakanusha Mitume.
142 Alipo waambia ndugu yao Saleh: Je! Hamumchimngu?
143 Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
144 Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit´iini.
145 Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
146 Je! Mtaachwa salama usalimina katika haya yaliyopo hapa?
147 Katika mabustani, na chemchem?
148 Na konde na mitende yenye makole yaliyo wiva.
149 Na mnachonga milimani majumba kwa ustadi.
150 Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit´iini mimi.
151 Wala msit´ii amri za walio pindukia mipaka,
152 Ambao wanafanya ufisadi katika nchi, wala hawatengenezi.
153 Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa walio rogwa.
154 Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi. Basi lete Ishara ukiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.
155 Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa, na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalumu.
156 Wala msimguse kwa uwovu, isije ikakushikeni adhabu ya Siku Kubwa.
157 Lakini wakamuuwa, na wakawa wenye kujuta.
158 Basi ikawapata adhabu. Hakika katika hayo ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
159 Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
160 Watu wa Lut´i waliwakanusha Mitume.
161 Alipo waambia ndugu yao, Lut´i: Je! Hamumchimngu?
162 Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu kwenu.
163 Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nit´iini mimi.
164 Wala mimi sikutakini ujira juu yake; ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
165 Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume?
166 Na mnaacha alicho kuumbieni Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnao ruka mipaka!
167 Wakasema: Ewe Lut´i! Usipo acha, hapana shaka utakuwa miongoni mwa wanao tolewa mji!
168 Akasema: Hakika mimi ni katika wanao kichukia hichi kitendo chenu.
169 Mola wangu Mlezi! Niokoe mimi na ahali zangu na haya wayatendayo.
170 Basi tukamwokoa yeye na ahali zake wote,
171 Isipo kuwa kikongwe katika walio kaa nyuma.
172 Kisha tukawaangamiza wale wengine.
173 Na tukawanyeshea mvua, basi ni ovu mno mvua ya waliyo onywa.
174 Hakika katika hayo ipo Ishara. Na hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
175 Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
176 Watu wa Machakani waliwakanusha Mitume.
177 Shuaibu alipo waambia: Je! Hamfanyi mkamchamngu?
178 Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
179 Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit´iini mimi.
180 Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
181 Timizeni kipimo sawa sawa, wala msiwe katika wanao punja.
182 Na pimeni kwa haki iliyo nyooka;
183 Wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye jeuri kwa ufisadi.
184 Na mcheni aliye kuumbeni nyinyi na vizazi vilivyo tangulia.
185 Wakasema: Hakika wewe ni katika walio rogwa.
186 Na wewe si chochote ila ni mtu tu kama sisi, na kwa yakini tunakuona wewe ni katika waongo.
187 Hebu tuangushie vipande kutoka mbinguni ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.
188 Akasema: Mola wangu Mlezi anajua zaidi mnayo yatenda.
189 Basi walimkanusha, na ikawashika adhabu ya siku ya kivuli. Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya siku kubwa.
190 Hakika katika hayo ipo Ishara, lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
191 Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
192 Na bila ya shaka hii ni Uteremsho wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
193 Ameuteremsha Roho muaminifu,
194 Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji,
195 Kwa ulimi wa Kiarabu ulio wazi.
196 Na hakika bila ya shaka haya yamo katika Vitabu vya kale.
197 Je! Haikuwa kwao ni Ishara kwamba wanayajua haya wanazuoni wa Wana wa Israili?
198 Na lau kuwa tungeli iteremsha juu ya mmoja wa wasio kuwa Waarabu,
199 Na akawasomea, wasingeli kuwa wenye kuamini.
200 Namna hivi tunaingiza katika nyoyo za wakosefu.
201 Hawataiamini mpaka waione adhabu chungu.
202 Basi itawafikia kwa ghafla, na hali hawana khabari.
203 Na watasema: Je, tutapewa muhula?
204 Basi, je, wanaihimiza adhabu yetu?
205 Waonaje kama tukiwastarehesha kwa miaka,
206 Kisha yakawafikia waliyo kuwa wakiahidiwa,
207 Yatawafaa nini yale waliyo stareheshewa?
208 Wala hatukuangamiza mji wo wote ila ulikuwa na waonyaji -
209 Kuwa ni ukumbusho. Wala Sisi hatukuwa wenye kudhulumu.
210 Wala Mashet´ani hawakuteremka nayo,
211 Wala haitakiwi kwao, na wala hawawezi.
212 Hakika hao wametengwa na kusikia.
213 Basi usimwombe mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakao adhibiwa.
214 Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe.
215 Na watwae kwa upole wanao kufuata miongoni mwa Waumini.
216 Na ikiwa watakuasi basi sema: Mimi najitenga mbali na hayo mnayo yatenda.
217 Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
218 Ambaye anakuona unapo simama,
219 Na mageuko yako kati ya wanao sujudu.
220 Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua.
221 Je! Nikwambieni nani wanawashukia Mashet´ani?
222 Wanamshukia kila mzushi mkubwa mwingi wa dhambi.
223 Wanawapelekea yale wanayo yasikia; na wengi wao ni waongo.
224 Na watungaji mashairi ni wapotofu ndio wanawafuata.
225 Je! Huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde?
226 Na kwamba wao husema wasiyo yatenda?
227 Isipo kuwa wale walio amini, na wakatenda mema, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi, na wakajitetea wanapo dhulumiwa. Na wanao dhulumu watakuja jua mgeuko gani watakao geuka.