37

1 Naapa kwa wanao jipanga kwa safu.
2 Na kwa wenye kukataza mabaya.
3 Na kwa wenye kusoma Ukumbusho.
4 Hakika Mungu wenu bila ya shaka ni Mmoja.
5 Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na yaliyomo kati yao, na ni Mola Mlezi wa mashariki zote.
6 Hakika Sisi tumeipamba mbingu ya karibu kwa pambo la nyota.
7 Na kulinda na kila shet´ani a´si.
8 Wasiweze kuwasikiliza viumbe watukufu. Na wanafukuzwa huko kila upande.
9 Wakifurushwa. Na wanayo adhabu ya kudumu.
10 Isipo kuwa anaye nyakua kitu kidogo, na mara humfwatia kimondo kinacho ng´ara.
11 Hebu waulize: Je! Wao ni wenye umbo gumu zaidi au hao wengine tulio waumba. Hakika Sisi tuliwaumba wao kwa udongo unao nata.
12 Bali unastaajabu, na wao wanafanya maskhara.
13 Na wanapo kumbushwa hawakumbuki.
14 Na wanapo ona Ishara, wanafanya maskhara.
15 Na husema: Haya si chochote ila ni uchawi tu ulio dhaahiri.
16 Ati tukisha kufa na tukawa udongo na mifupa ndio kweli tutafufuliwa?
17 Hata baba zetu wa zamani?
18 Sema: Naam! Hali nanyi ni madhalili.
19 Huko utapigwa ukelele mmoja tu! Na hapo ndio wataona!
20 Watasema: Ole wetu! Hii ndiyo Siku ya Malipo.
21 Hii ndiyo Siku ya Hukumu mliyo kuwa mkiikadhibisha.
22 Wakusanyeni walio dhulumu, na wake zao, na hao walio kuwa wakiwaabudu -
23 Badala ya Mwenyezi Mungu. Waongozeni njia ya Jahannamu!
24 Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa:
25 Mna nini? Mbona hamsaidiani?
26 Bali hii leo, watasalimu amri.
27 Watakabiliana wao kwa wao kuulizana.
28 Watasema: Kwa hakika nyinyi mlikuwa mkitujia upande wa kulia.
29 Watasema (wakubwa): Bali nyinyi wenyewe hamkuwa Waumini.
30 Sisi hatukuwa na mamlaka juu yenu, bali nyinyi wenyewe mlikuwa wapotovu.
31 Basi hukumu ya Mola wetu Mlezi imekwisha tuthibitikia. Hakika bila ya shaka tutaonja tu adhabu.
32 Tulikupotezeni kwa sababu sisi wenyewe tulikuwa wapotovu.
33 Basi wao kwa hakika siku hiyo watashirikiana katika adhabu pamoja.
34 Hivyo ndivyo tutakavyo wafanyia wakosefu.
35 Wao walipo kuwa wakiambiwa La ilaha illa ´Llahu Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu tu, wakijivuna.
36 Na wakisema: Hivyo sisi tuiache miungu yetu kwa ajili ya huyu mtunga mashairi mwendawazimu?
37 Bali huyu amekuja kwa Haki, na amewasadikisha Mitume.
38 Hakika nyinyi bila ya shaka mtaionja adhabu chungu.
39 Wala hamlipwi ila hayo mliyo kuwa mkiyafanya.
40 Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa.
41 Hao ndio watakao pata riziki maalumu,
42 Matunda, nao watahishimiwa.
43 Katika Bustani za neema.
44 Wako juu ya viti wamekabiliana.
45 Wanazungushiwa kikombe chenye kinywaji cha chemchem
46 Kinywaji cheupe, kitamu kwa wanywao.
47 Hakina madhara, wala hakiwaleweshi.
48 Na watakuwa nao wanawake wenye macho ya staha mazuri.
49 Hao wanawake kama mayai yaliyo hifadhika.
50 Waingie kuulizana wenyewe kwa wenyewe.
51 Aseme msemaji mmoja miongoni mwao: Hakika mimi nalikuwa na rafiki
52 Aliye kuwa akinambia: Hivyo wewe ni katika wanao sadiki
53 Ati tukisha kufa tukawa udongo na mafupa, ndio tutalipwa na kuhisabiwa?
54 Atasema: Je! Nyie mnawaona?
55 Basi atachungulia amwone katikati ya Jahannamu.
56 Atasema: Wallahi! Ulikaribia kunipoteza.
57 Na lau kuwa si neema ya Mola wangu Mlezi bila ya shaka ningeli kuwa miongoni mwa walio hudhurishwa.
58 Je! Sisi hatutakufa,
59 Isipo kuwa kifo chetu cha kwanza? Wala sisi hatutaadhibiwa.
60 Hakika huku bila ya shaka ndiko kufuzu kukubwa.
61 Kwa mfano wa haya nawatende watendao.
62 Je! Kukaribishwa hivi si ndio bora, au mti wa Zaqqum?
63 Hakika Sisi tumeufanya huo kuwa ni mateso kwa walio dhulumu.
64 Hakika huo ni mti unao toka katikati ya Jahannamu.
65 Mashada ya matunda yake kama kwamba vichwa vya mashet´ani.
66 Basi hakika bila ya shaka hao watayala hayo, na wajaze matumbo.
67 Kisha juu yake wanyweshwe mchanganyo wa maji yamoto yaliyo chemka.
68 Kisha hakika marejeo yao bila ya shaka yatakuwa kwenye Jahannamu.
69 Hakika waliwakuta baba zao wamepotea.
70 Na wao wakafanya haraka kufuata nyayo zao.
71 Na bila ya shaka walikwisha potea kabla yao wengi wa watu wa zamani.
72 Na Sisi hakika tuliwapelekea waonyaji.
73 Basi hebu angalia ulikuwaje mwisho wa walio onywa.
74 Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa.
75 Na hakika Nuhu alitwita, na Sisi ni bora wa waitikiaji.
76 Na tulimwokoa yeye na ahali zake kutokana na msiba mkubwa.
77 Na tuliwajaalia dhuriya zake ndio wenye kubakia.
78 Na tukamwachia (sifa njema) kwa walio kuja baadaye.
79 Iwe salama kwa Nuhu ulimwenguni kote!
80 Kwa hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema.
81 Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini.
82 Kisha tukawazamisha wale wengine.
83 Na hakika Ibrahim alikuwa katika kundi lake,
84 Alipo mjia Mola wake Mlezi kwa moyo mzima.
85 Alimwambia baba yake na watu wake: Mnaabudu nini?
86 Kwa kuzua tu mnataka miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu?
87 Mnamdhania nini Mola Mlezi wa walimwengu wote?
88 Kisha akapiga jicho kutazama nyota.
89 Akasema: Hakika mimi ni mgonjwa!
90 Nao wakamwacha, wakampa kisogo.
91 Basi akaiendea miungu yao kwa siri, akaiambia: Mbona hamli?
92 Mna nini hata hamsemi?
93 Kisha akaigeukia kuipiga kwa mkono wa kulia.
94 Basi wakamjia upesi upesi.
95 Akasema: Hivyo mnaviabudu vitu mnavyo vichonga wenyewe?
96 Na hali Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni nyinyi na hivyo mnavyo vifanya!
97 Wakasema: Mjengeeni jengo, na kisha mtupeni motoni humo!
98 Basi walitaka kumfanyia vitimbi, lakini tukawafanya wao ndio wa chini.
99 Na akasema: Hakika mimi nahama, nakwenda kwa Mola wangu Mlezi; Yeye ataniongoa.
100 Ewe Mola wangu Mlezi! Nitunukie aliye miongoni mwa watenda mema.
101 Basi tukambashiria mwana aliye mpole.
102 Basi alipo fika makamo ya kwenda na kurudi pamoja naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyo amrishwa, utanikuta mimi, Inshallah, katika wanao subiri.
103 Basi wote wawili walipo jisalimisha, na akamlaza juu ya kipaji.
104 Tulimwita: Ewe Ibrahim!
105 Umekwisha itimiliza ndoto. Hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao tenda mema.
106 Hakika haya ni majaribio yaliyo dhaahiri.
107 Basi tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu.
108 Na tukamwachia (sifa njema) kwa watu walio kuja baadaye.
109 Iwe salama kwa Ibrahim!
110 Hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema.
111 Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini.
112 Na tukambashiria kuzaliwa Is-haqa, naye ni Nabii miongoni mwa watu wema.
113 Na tukambarikia yeye na Is-haqa. Na miongoni mwa dhuriya zao walitokea wema na wenye kudhulumu nafsi zao waziwazi.
114 Na kwa hakika tuliwafanyia hisani Musa na Haruni.
115 Na tukawaokoa wao na watu wao kutokana na dhiki kubwa.
116 Na tukawanusuru; na wakawa wao ndio wenye kushinda.
117 Na tukawapa wawili hao Kitabu kinacho bainisha.
118 Na tukawaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka.
119 Na tukawaachia (sifa njema) katika watu walio kuja baadaye.
120 Iwe salama kwa Musa na Haruni!
121 Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema.
122 Hakika wawili hao ni katika waja wetu walio amini.
123 Na hakika Ilyas bila ya shaka alikuwa miongoni mwa Mitume.
124 Alipo waambia watu wake: Hamwogopi?
125 Mnamwomba Baa´li na mnamwacha Mbora wa waumbaji,
126 Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa zamani?
127 Wakamkadhibisha. Basi kwa hakika watahudhurishwa;
128 Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa.
129 Na tumemwachia (sifa nzuri) kwa walio kuja baadaye.
130 Iwe salama kwa Ilyas.
131 Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema.
132 Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini.
133 Na hakika Lut´i bila ya shaka ni miongoni mwa Mitume.
134 Tulipo mwokoa yeye na ahali zake wote,
135 Isipo kuwa mwanamke mkongwe katika wale walio bakia nyuma.
136 Kisha tukawaangamiza wale wengineo.
137 Na hakika nyinyi mnawapitia wakati wa asubuhi,
138 Na usiku. Basi je! Hamyatii akilini?
139 Na hakika Yunus alikuwa miongoni mwa Mitume.
140 Alipo kimbia katika jahazi lilio sheheni.
141 Akaingia katika kupigiwa kura, na akawa katika walio shindwa.
142 Samaki akammeza hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa.
143 Na ingeli kuwa hakuwa katika wanao mtakasa Mwenyezi Mungu,
144 Bila ya shaka angeli kaa ndani yake mpaka siku ya kufufuliwa.
145 Lakini tulimtupa ufukweni patupu, hali yu mgonjwa.
146 Na tukauotesha juu yake mmea wa kabila ya mung´unye.
147 Na tulimtuma kwa watu laki moja au zaidi.
148 Basi wakaamini, na tukawastarehesha kwa muda.
149 Basi waulize: Ati Mola wako Mlezi ndiye mwenye watoto wa kike, na wao wanao watoto wa kiume?
150 Au tumewaumba Malaika kuwa ni wanawake, na wao wakashuhudia?
151 Ati ni kwa uzushi wao ndio wanasema:
152 Mwenyezi Mungu amezaa! Ama hakika bila ya shaka hao ni waongo!
153 Ati amekhiari watoto wa kike kuliko wanaume?
154 Mna nini? Mnahukumu vipi nyinyi?
155 Hamkumbuki?
156 Au mnayo hoja iliyo wazi?
157 Basi leteni Kitabu chenu kama mnasema kweli.
158 Na wameweka makhusiano ya nasaba baina yake na majini; na majini wamekwisha jua bila ya shaka kuwa wao watahudhurishwa.
159 Subhana ´Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo msingizia.
160 Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa.
161 Basi hakika nyinyi na mnao waabudu
162 Hamwezi kuwapoteza
163 Isipo kuwa yule atakaye ingia Motoni.
164 Na hapana katika sisi ila anapo mahali pake maalumu.
165 Na hakika bila ya shaka sisi ndio wajipangao safu.
166 Na hakika sisi ndio wenye kusabihi kutakasa.
167 Na walikuwapo walio kuwa wakisema:
168 Tungeli kuwa na Ukumbusho kama wa watu wa zamani,
169 Bila ya shaka tungeli kuwa ni waja wa Mwenyezi Mungu wenye ikhlasi.
170 Lakini waliukataa. Basi watakuja jua.
171 Na bila ya shaka neno letu lilikwisha tangulia kwa waja wetu walio tumwa.
172 Ya kuwa wao bila ya shaka ndio watakao nusuriwa.
173 Na kwamba jeshi letu ndilo litakalo shinda.
174 Basi waachilie mbali kwa muda.
175 Na watazame, nao wataona.
176 Je! Wanaihimiza adhabu yetu?
177 Basi itakapo shuka uwanjani kwao, itakuwa asubuhi mbaya kwa walio onywa.
178 Na waache kwa muda.
179 Na tazama, na wao wataona.
180 Subhana Rabbi´l´Izzat Ametakasika Mola Mlezi Mwenye enzi na yale wanayo mzulia.
181 Na Salamu juu ya Mitume.
182 Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote.